Exodus 18

Yethro Amtembelea Musa

1 aBasi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Musa, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Musa na watu wake wa Israeli, pia jinsi Bwana alivyowatoa Israeli Misri.

2 bBaada ya Musa kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea 3 cpamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Musa alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” 4 dMwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”

5 eYethro, baba mkwe wa Musa, pamoja na wana wawili wa Musa na mkewe, wakamjia Musa huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu. 6Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Musa, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”

7 fKwa hiyo Musa akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. 8 gMusa akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Bwana alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsi Bwana alivyowaokoa.

9 hYethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuri Bwana aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri. 10 iYethro akasema, “Sifa na ziwe kwa Bwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri. 11 jSasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.” 12 kKisha Yethro, baba mkwe wa Musa, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Haruni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Musa mbele za Mungu.

Ushauri Wa Yethro

(Kumbukumbu 1:9-18)

13Siku iliyofuata, Musa akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. 14Baba mkwe wake alipoona yote Musa anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”

15 lMusa akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. 16 mKila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.”

17Baba mkwe wa Musa akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. 18 nWewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. 19 oSasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. 20 pUwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya. 21 qLakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 22 rWaweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. 23Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”

Kuchaguliwa Kwa Waamuzi

24Musa akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. 25 sMusa akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 26 tWakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Musa, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.

27 uKisha Musa akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.
Copyright information for SwhKC